Wito wa Usaili Kushiriki Mradi wa Vijana Kilimo Biashara

Vijana Kilimo Biashara (VKB) ni mradi bunifu unaowawezesha vijana wajasiriamali katika mikoa ya Dodoma na Singida kuleta suluhisho endelevu kwenye sekta ya kilimo. Kupitia mafunzo, ushauri, na upatikanaji wa rasilimali, VKB inasaidia biashara zinazomilikiwa na vijana zinazolenga kuongeza uzalishaji, kupunguza upotevu wa mazao, na kuimarisha mifumo ya masoko kwa mazao kama mtama, alizeti, na mazao ya bustani. Vijana wenye biashara au ubunifu katika kilimo wanaweza kujiandikisha bure kwa kubonyeza hapa kabla ya tarehe 20 Novemba 2024 ili kushiriki katika fursa hii ya kipekee ya kujenga ustadi na kuchangia ukuaji wa mifumo ya chakula yenye ustahimilivu.

A woman voicing her opinion in a cooperative meeting

Deadline:

November 20, 2024

Wito wa Usaili Kushiriki Mradi wa Vijana Kilimo Biashara

Je, wewe ni mjasiriamali kijana na mwenye shauku ya kuunda suluhisho jipya lenye ubunifu ili kuhakikisha uendelevu na ujumuishi katika mifumo ya usalama na chakula kutoka mkoa wa Dodoma au Singida? Je, unayo biashara au ubunifu unaoongeza thamani katika mnyororo wa zao la mtama, alizeti au kilimo cha mbogamboga na matunda? Je, wewe ni kijana mwenye msukumo wa shughuli za kilimobiashara, au mtoa huduma mwenye maono, mtendaji kazi mbunifu, au labda wewe kijana unayetoa huduma za chakula na lishe?

Wakati wako ni sasa, Jisajili na upate nafasi ya kushiriki kwenye mradi wa Vijana Kilimo Biashara (VKB)! Kwa sasa tunatafuta vijana wa kike na kiume ambao ni wajasiriamali na wanaofanya biashara mbalimbali zinazojihusisha katika mnyororo wa thamani wa kilimo cha zao la alizeti na mtama pamoja na mazao ya bustani (mbogamboga na matunda). Fursa hii ni nafasi yako ya wewe kuweza kujisajili na kushiriki katika mradi wa Vijana Kilimo Biashara, ili uwezweze kupata uwezeshaji wa kibiashara na hatimaye kuchangia kikamilifu katika mfumo endelevu wa chakula unaojumuisha watu wote.

Mradi wa VKB unahusika na nini na unamelengo yapi?

Vijana Kilimo Biashara (VKB) ni mradi wa vijana unaolenga kuongeza kiwango cha uzalishaji na kupunguza upotevu wa mazao ya mtamana alizeti baada ya mavuno, ikiwa pamoja na kuongeza fursa za ajira kwa Vijana na upatikanaji wa masoko. mradi huu unaotekelezwa katika mkoa wa Dodoma na Singida unaosimami na kuendeshwa na shirika la Rikolto Africa Mashariki kwa kushirikiana na AgriHub Tanzania, Inades Formation Tanzania, 360 Connect na Flying Dream kupitia ufadhili wa Shirikika la Chakula Duniani la Umoja wa Mataifa (WFP) na MasterCard Foundation.

Vijana Kilimo Biashara ni mradi uliojikita katika kuibua na kuboresha biashara bunifu zinazolenga kutoa huduma suluhishi katika changamoto zilizopo kwenye mnyororo wa thamani wa mifumo ya chakula na masoko kutoka mkoa wa Dodoma na Singida. Mradi huu unakusudia kutambua na kuendeleza vijana wajasiriamali na wabunifu wenye biashara zinazoweza kuendeleza na kukuza usawa wa mnyororo wa thamani wa mifumo ya chakula nchini Tanzania. Mradi huu unatarajia kusaili biashara mia moja (100), biashara hamsini (50) kutoka kila upande wa mkoa wa Dodoma na Singida na kuwa wanufaika wa mradi. Katika mradi huu, washiriki watapata mafunzo ya kina kuhusu: urasimishaji wa bashara, ubunifu wa mtindo/muundo wa kibiashara, chapa na alama za biashara pamoja na utafutaji na ushindani wa masoko, masuala ya kodi na taratibu za kisheria kuhusiana na biashara, pia watapata nafasi ya kukutana na wataalamu kutoka taasisi mbalimbali, pamoja wajasiriamali waliofanikiwa katika sekta na wanaotokea kwenye mazingira yao.

Mradi wa VKB unalenga kuwezesha biashara zipi?

Mradi unatarajia kusaili vijana wajasiriamali na wenye biashara bunifu zinalolenga kutatua changamoto kutoka katika maeneo makuu 3 yanayopewa kipaumbele;

1. Kuongeza kiwango cha uzalishaji endelevu na salama kwa kilimo cha zao la alizeti, mtama au mbogamboga na matunda kwa kuongeza ujumuishi wa kifedha kwa upatikanaji wa mitaji rafiki na nafuu kwa wakulima wadogo, kutoa huduma za ugani kitaalamu na kuunda teknolojia bunifu zinazoweza kuongeza tija katika matumizi ya kanuni bora za kilimo (mf. matumizi ya mbegu bora, mashine za kupandia mbegu, palizi au uvunaji. Pamoja na utengenezaji wa mifumo husishi ya udhibiti wa visumbufu (wadudu na magonjwa) kwenye mazao pamoja na upimaji wa afya ya udongo, matumizi ya chokaa mazao na urutubishaji wa udongo, matumizi sahihi ya mbolea na viuatilifu vya kuua wadudu waharibifu na magonjwa ya mimea, vifaa vya umwagiliaji kwa kutumia nishati ya jua, teknolojia bunifu za kilimo hifadhi/hai/rejea au Kilimo stahimilivu dhidi ya mabadiliko ya tabia nchi)

2. Kupunguza kiwango cha upotevu wa mazao baada ya mavuno, kwa kutoa suluhisho la ubunifu ama teknolojia za utunzaji au uhifadhi endelevu na salama wa mazao ya mtama na alizeti mara baada ya mavuno au kwenye mnyororo wote wa thamani baada ya mavuno, hususani kupunguza kiwango cha upotevu wa ubora, kiasi au thamani; katika hatua ya uvunaji, ukaushaji, uchambuaji, upigaji, upukuchuaji au kupura, usafishaji, upepetaji, uchakataji, usindikaji, ufungashaji, uhifadhi, usafirishaji na hata kwenye usambazaji wa mazao ya alizeti na mtama au mbogamboga na matunda (mf. teknolijia za uvunaji na ukusanyaji wa mazao kutoka kwa wakulima, kupiga au kupura mavuno kwa mashine, uhifadhi maghalani, kwenye mifuko ya kinga njaa, uongezaji wa thamani wa mazao ya alizeti na mtama na kupata bidhaa nzuri na bora zinazokidhi mahitaji au matumizi ya walaji wa mwisho, kama vile utengenezaji wa malisho ya mifugo na ujumuishi wa vyakula au kuhakikisha upatikanaji wa vyakula vyenye afya na lishe kwa watu wote, ikiwa pamoja na utoaji wa lishe bora mashuleni)

3. Kuimarisha na kustawisha mifumo ya masoko (ununuzi na uuzaji) wenye tija kwa bidhaa na huduma zinazohitajika kwa wateja au wakulima wa zao la alizeti na mtama pamoja na mazao ya bustani; pia kuwezesha uunganishwaji wa wadau wanaohusika kwenye mnyororo mzima wa thamani kuanzia kwenye pembejeo za uzalishaji, teknolojia za kilimo na uhifadhi wa mazao baada ya mavuno, uchakataji na usindikaji wa bidhaa za mazao husika, pamoja na usafirishaji na usambazaji hadi kwa walaji wa mwisho (mf. kuendeleza biashara za uuzaji wa pembejeo za kilimo, ununuzi na uuzaji wa mazao kupitia vituo maalumu vya kukusanyia mazao, uuzaji wa vifungashio, na bidhaa zenye ubora zilizo ongezewa thamani, pamoja na utoaji wa huduma maalumu na/ama za muhimu zinazohitajika kwa wakulima wadogo wadogo wa mazao husika)

Mtiririko wa Mradi wa Vijana Kilimo Biashara (VKB)

Mradi unalenga kufanya uwezeshaji wa vijana kibiashara kwa moduli mbalimbali    kupitia katika hatua zifuatazo kuanzia mwanzo hadi mwisho wa mradi huu.

a. Kufunguliwa kwa dirisha la usaili na kuhamasisha ushiriki wa vijana

• Kuhamashisha vijana kujitokeza kushiriki kupitia Halmashauri zao

• Kupokea maombi ya usaili, mwisho wa kufunga Tarehe: 20.11.2024

b. Mafunzo kambini kwa washiriki wa mkoa wa Dodoma na Singida

• Biashara 100 (50 kila mkoa) zitachaguliwa, kupatiwa mafunzo ya kina

• Siku 7 za mafunzo ya kina kwa kila mkoa, juu ya ubunifu na elimu ya    uendelezaji biashara pamoja na kukutana na wataalamu mbalimbali.

c. Uwezeshaji wa ushauri na malezi ya kibiashara

• Biashara 50 (Biashara 25 kila mkoa) zitachaguliwa kwa uwezeshaji wa                     malezi na ushauri binafsi wa uendelezaji biashara kwa muda wa miezi 3

• Uandaaji wa mchanganuo wa mpango biashara na utafiti wa masoko.

• Mafunzo binafsi na ushauri wa kibiashara wa kujiandaa na uwekezaji.

• Uunganishwaji na taasisi za kifedha, masoko na wadau muhimu.

d. Fainali: Siku ya maonesho ya ubunifu na uzinduzi wa bishara mpya

• Biashara 20 (Biashara 10 kila mkoa) kupata mtaji hadi Tsh.70,000,000

• Fursa ya kuzindua kampuni mpya za kibiashara mbele ya wadau.

• Fursa ya kukutana na watalaamu na wafanyabiashara mbalimbali.

• Fursa ya kujitangaza kibiashara, kufahamiana na washirika wengine.

• Fursa ya kukuza mtaji kibiashara ama kuungana na wadau wengine.

Nani anaweza kushiriki mradi huu wa VKB?

Kijana yeyote ambaye anasifa zinazostahiki kushiriki ikiwa endapo kama;

• Wewe ni binti au kijana wa kiume mwenye umri kati ya miaka 18-35

• Wajasiriamali wanawake wanapewa kipaumbele kushiriki mradi huu

• Unatoka katika vijiji au maeneo ya mkoa wa Dodoma katika wilaya zifuatazo: Dodoma, Chamwino, Kongwa, Mpwapwa, Bahi, Chemba na Kondoa au kutoka mkoa wa Singida katika wilaya zifuatazo: Singida Mjini, Singida Vijijini, Manyoni, Itigi, Mkalama, Iramba na Ikungi.

• Tayari unamiliki ubunifu, bidhaa/sampuli kifani au umesha anzisha biashara inayozalisha bidhaa au inayotoa huduma katika mnyororo wa thamani wa mazao ya mtama na alizeti au mazao ya bustani.

• Unabiashara au ubunifu unaolenga kutatua changamoto kwa wakulima wadogo na zilizopo katika mnyororo wa thamani wa alizeti na mtama

• Unabiashara au ubunifu unayoweza kutoa fursa za ajira kwa wanawake na vijana wengine na inayoonesha matarajio ya ukuaji zaidi

• Unashauku ya kukuza na kuendeleza biashara hasa kwenye mnyororo wa thamani wa mazao ya mtama, alizeti au mazao ya bustani.

• Ukichaguliwa utakuwa tayari kushiriki kikamilifu bila kukosa katika kipindi chote cha mradi wa VKB mpaka kuhitimishwa kwake.

Je, umevutiwa na mradi huu wa VKB?

Jiandikishe au jisajili sasa! Kushiriki ni bure kabisa.

Kwa namna gani naweza kujisajili?

Ingia kwenye kiunganishi hiki cha mtandao au link hii: https://bit.ly/VKB-GFA kisha jaza fomu na uiwasilishe, mwisho Tarehe 20 November 2024. Endapo kama unakutana na changamoto katika kujiandikisha tafadhali wasiliana na waratibu wa mradi kupitia barua pepe: agrihubtanzania@gmail.com au wasiliana kwa simu nambari: +255 787 220 120

Endelea kufuatilia mradi huu kupitia kurasa zetu za Instagram na Facebook au kwa kutufuatilia kwa jina la: @generationfood.tanzania #GenerationFoodAccelerator

Ni nini kinachoweza kutokidhi sifa za usaili huu?

Sababu zinazoweza kupelekea maombi kukosa nafasi ya usaili wa kushiriki katika mradi huu ni pamoja na mambo haya yafuatayo;

1. Maombi yasiyoweza kuonesha ubunifu wenye tija au kushindwa kueleza changamoto inayotatuliwa, au kuelezea suluhisho la tatizo kwa kutumia mbinu za kizamani lakini zisizo onesha ubunifu mpya unaweza kuongeza thamani/utofauti wa kipekee.

2. Maombi yasiyo lenga au yasiyoendana na shabaha ya mradi huu.

3. Maombi yanayotoa pendekezo au wazo la kuanzisha biashara ambayo haipo.

4. Maombi yasiyoweza kujibu maswali yote kiukamilifu, kwa usahihi na ufasaha.

5. Waombaji wasio na sifa zinazostahiki kushiriki katika mradi huu kama zilivyotajwa.

Vigezo gani vinavyotumika katika usahili wa VKB?

Washiriki wote watakaotuma maombi yao watachaguliwa kwa vigezo sawa kupitia kanuni ya ushindani, hivyo kila mshiriki anapaswa kufahamu vigezo vitakavyotumika kama ifuatavyo:

1. Tatizo au changamoto (25%) muombaji hanabudi kueleza bayana juu ya changamoto ama

tatizo aliloliona katika maeneo 3 yanayopewa kipaumbele. tatizo linawaathiri watu gani na kwa wingi kiasi gani? wakati gani zaidi ambapo tatizo hutokea na wapi? madhara ni yapi?

2. Suluhisho au ubunifu (25%) muombaji anatakiwa kueleza mbinu, dhana ama ubunifu upi

unaoweza kung’amua tatizo/changamoto iliyotajwa? endapo suluhisho lisipotekelezwa/kuwezeshwa kuna madhara yapi?

3. Soko au watumiaji (20%) suluhisho la ubunifu lina watumiaji au wateja gani? wapo

wapi? na suluhisho linaweza kufikia kiasi gani cha watumiaji? wateja wanaweza kutumia ama kununua kwa garama kiasi gani? ni misimu ipi auwakati gani suluhisho linahitajika zaidi?

4. Mtindo wa biashara (15%) kwa namna gani ubunifu unaweza kuwa biashara na kuingiza

Kipato? bidhaa au huduma zipi zinazoweza kuzalishwa? kuna mbinu zipi za uuzaji/namna wateja wanavyoweza kufikiwa?

5. Umuhimu wake/uliopo (15%) ubunifu unaweza kuwa na tija gani katika kuleta fursa za

ajira na ushirikishwaji wa vijana na wanawake? Je, kuna tija katika kutatua changamoto kijamii, kiuchumi na mazingira?

Kalenda ya matunio muhimu ya mradi wa VKB

Tarehe: 08 – 15 Nov 2024 Kuhamasisha washiriki kupitia kwenye Halmashauri zao

Tarehe: 10 – 20 Nov 2024 Ufunguzi wa dirisha la maombi ya ushiriki wa mradi

Tarehe: 20 – 20 Nov 2024 Kufungwa kwa dirisha la kupokea maombi ya washiriki

Tarehe: 22 – 26 Nov 2024 Kuhakiki maombi ya vijana na kuchagua wa washiriki

Tarehe: 27 – 29 Nov 2024 Kutoa taarifa kwa washiriki waliochaguliwa katika mradi

Tarehe: 01 – 07 Dec 2024 Wiki ya mafunzo kambini kwa washiriki wa mkoa wa Dodoma

Tarehe: 08 – 14 Dec 2024 Wiki ya mafunzo kambini kwa washiriki wa mkoa wa Singida

Tarehe: 16 – 30 Dec 2024 Kuhakiki biashara za washiriki na kuzitathmini mahitaji yake

Tarehe: 1/01–30/03 2025 Malezi na ushauri elekezi wa kibiashara kwa wanufaika

Tarehe: 10–20 Aprili 2025 Fainali na utoaji wa tuzo kwa washindi wa mradi wa VKB

Kwa namna gani naweza kujisajili?

Ingia kwenye kiunganishihiki cha mtandao au link hii: https://bit.ly/VKB-GFA kisha jaza fomu na uiwasilishe, mwisho Tarehe 20 November 2024. Endapo kama unakutana na changamoto katika kujiandikisha tafadhali wasiliana na waratibu wa mradi kupitia barua pepe: agrihubtanzania@gmail.com au wasiliana kwa simu nambari: +255 787 220 120

 

Endelea kufuatilia mradi huu kupitia kurasa zetu za Instagram na Facebook au kwa kutufuatilia kwa jina la: @generationfood.tanzania#GenerationFoodAccelerator